Jinsi Ya Kupika UROJO
Urojo ni mchanganyiko wa vyakula mbali mbali pamoja na uji uji wake katika bakuli moja.
Hapa nitaeleza jinsi ya kuupika huo uji(urojo) mpaka kukamilika kwake.
Asili ya urojo ni India ila kwa sasa nchi mbali mbali zina andaa upishi huu.
Na Zanzibar ni mlo unaopendwa na maarufu sana.Na hii ndio aina ya urojo unaopikwa Zanzibar.
Kwenye Urojo Tunaweka
1.Mbatata za Kuchemsha
2.Mayai Ya Kuchemsha
3.Badia
4.Chatne
MAHITAJI
1.Unga wa Ngano Mug 1
2.Ndimu zilokamuliwa 2
3.Maji Lita 2
4.Chumvi Kiasi
5.Bizari Kijiko cha chai 1
MAANDALIZI
1.Weka unga kwenye bakuli kisha weka maji nusu lita pamoja na bizari.
2.Koroga hadi uhakikishe mabonge yote yameisha.
JINSI YA KUPIKA
1.Mimina maji Yalobakia kwenye sufuria weka chumvi kiasi acha yachemke sana.
2.Kisha mimina uji wenye bizari kwenye maji ya moto taratibu huku ukikoroga mpaka uchanganyike.
3.Acha uchemke kidogo kisha mimina ndimu yako na ukoroge kidogo.
4.Acha uchemke onja chumvi na ndimu kama zipo sawa epua.
5.Ikiwa urojo ni mzito sana ongeza maji acha uchemke kidogo kisha uepue.
Angalizo:
1.Kama urojo ukiwa mkali au una chumvi nyingi ongeza maji kidogo kidogo mpaka upungue ukali.
2.Hakikisha huuachi jikoni kwa muda mrefu mpaka ukaungua.
3.Usiweke maji mengi ukawa mwepesi kupitiliza.
Jinsi ya Kuuandaa
1.Menya Viazi Mbatata ulivyovichemsha kisha vipasue kati na vikate vipande vidogo vidogo.
2.Menya Mayai yaliochemshwa na yapasue kati na kata vipande vinne.
3.Chukua Bakuli na kijiko.
4.Weka vipande vya viazi ulivyovikata katika kibakuli chenye kijiko.
5.Weka na vipande vya mayai kwenye bakuli.
6.Malizia kuweka kachori,badia,mishkaki,chipsi za muhogo na katlesi.
7.Kisha mimina urojo kiasi upendacho.
8.Weka chatne na pilipili.
9.Upo tayari kuliwa wenyewe au na mkate upendao na kinywaji upendacho.