Rais wa Marekani Donald Trump Akosolewa
Rais wa Marekani Donald Trump amekumbana na ukosoaji mkali baada ya kauli zake za utata dhidi ya rais wa Ukraine Volodomir Zelenskyy.
Trump ameshambuliwa vikali na wafuasi wake ikiwemo raia wa Marekani ambao wamesema kwa kauli yake kwamba Ukraine ndio imeanzisha vita dhidi ya Urusi wanajuta kumchagua na wanaona aibu kuwa Wamarekani.
Kauli ya Trump imekosolewa vikali mno ulimwenguni kote ikiwemo kwenye majukwaa ya kijamii hususan mtandao wa X ambapo taarifa rasmi za utafiti zimeonesha rais Volodomir Zelensky wa Ukraine bado anaungwa mkono kwa asilimia 52 na raia wa nchi yake takwimu ambazo zimebatilisha madai ya uongo ya rais Trump kwamba Zelensky anakubalika kwa asilimia 4 tu.
Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer ni kati ya viongozi wakubwa aliyejitokeza hadharani kumpinga vikali Trump na kumtetea Zelenskyy. Starmer amesema ni aibu kwa taifa lililovamiwa kushutumiwa kwamba ndio limeanzisha vita.
Starmer ametetea suala la Zelenskyy kuendelea kuwa rais akisema ni kawaida rais katika vita kuendelea kutawala kwakua hakuna nafasi ya kufanya uchaguzi akisema hata Uingereza ilishawahi kutokea hali kama hiyo.
Wafuasi wengi katika mitandao ya kijamii ya kurasa rasmi za rais Trump wamemporomoshea mvua ya matusi na masikitiko yao kufuatia kauli zake hizo ambazo wamedai hazijaangalia uhalisia wa vita hiyo.