Waasi nchini Kongo wazidi kusonga mbele mpaka Bukavu
Waasi nchini Kongo wamezidi kusonga mbele na sasa wanaushikilia mji wa pili kwa ukubwa wa Bukavu huko Kivu. Watu wanajiuliza ni kwanini Corneille Nangaa ndio kiongozi mkuu wa waasi hao na sio Sultan Makenga au Bertrand Bisimwa?
Nangaa ni mkongo halisi na msomi zaidi kati ya viongozi wa makundi hayo ya waasi pia ndio kiongozi wa waasi aliyewahi kushika madaraka makubwa zaidi katika serikali ya Kongo akiwa kama mwenyekiti wa tume ya Taifa ya Uchaguzi maarufu kama CENI na ndiye aliyemtangaza Felix Tshisekedi mshindi.
Kutokana na kashfa za M23 na waasi wengine kuungwa mkono na Rwanda, Nangaa amekua akisimama kama kiongozi mkuu wa makundi hayo ili kuua dhana hiyo maana viongozi wengine wana historia ya ukaribu mno na Rwanda.
Yanayoendelea Kongo ni dhahiri Majeshi ya serikali yamelemewa vibaya na sasa waasi kila mji wanaoingia vikosi vya serikali vinakimbia na kuondoka
Hii ni ishara mbaya kwamba kwa vyovyote vile serikali ya Kongo haijajipanga kumudu nguvu hii mpya ya waasi. Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Antonio Guteres ameonya uwezekano wa taifa hilo kugawanyika
Rais Felix Tshisekedi kwenye hili atajilaumu mwenyewe, toka ameingia Ikulu 2018 sijui alikuwa anafanya nini? Miaka zaidi ya mitano upo Ikulu umeshindwa kuunda jeshi imara kulinda nchi dhidi ya waasi? Nchi iliyojaa utajiri mkubwa wa madini?
Nangaa anasema mpango wa waasi kwa sasa ni kuitwaa Kinshasa na kwa mwendo ulivyo ni dhahiri Tshisekedi ana wakati mgumu kuliko wakati wowote sasa
Kwingineko Rwanda imesema haitishwi na vikwazo vya kiuchumi kuhusiana na mzozo wa mashariki mwa Kongo na tayari imetangaza kusitisha ushirikiano wa kiuchumi na Ubelgiji ambayo ilikuwa imesaini tayari msaada wa euro milioni 95 za msaada kwa Rwanda
Je Tshisekedi atafanikiwa kuwazuia waasi?
NB: This blog does not support rebels in DR Congo, it strictly condemns the ongoing war in Eastern DR Congo