Donald Trump atishia kuharibu uchumi wa Urusi
Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuharibu uchumi wa Urusi iwapo haitokubali mpango wa kusitisha vita hatua ya kwanza siku 30 uliowasilishwa kwake jana na wapatanishi kutoka Marekani baada ya kikao chao na wawakilishi wa juu wa Ukraine nchini Saudi Arabia.
Kauli ya Trump inafuata siku chache baada ya Marekani kurejesha misaada ya kijeshi na intelijensia kwa Ukraine huku Urusi ikisema urejeshwaji wa misaada ya kijeshi ya Marekani kwa Ukraine ni hatua ya kulaaniwa inayoendelea kuchochea vita.
Baada ya Marekani kusitisha misaada kwa Ukraine wiki mbili zilizopita Urusi ilitumia fursa hiyo kuongeza mashambulizi makali dhidi ya Ukraine jambo ambalo lilimuudhi mno rais wa Marekani Donald Trump na kubadili msimamo wake wa awali kuhusu kuzuia misaada ya kijeshi na intelijensia kwa Ukraine.
Baada ya mazungumzo na Ukraine nchini Saudi Arabia jana na juzi, serikali ya Marekani imesema sasa mpira upo mikononi mwa Urusi kuridhia mpango huo wa amani ambao Ukraine imeshakubali vinginevyo ikumbane na dhahama kubwa ya kiuchumi itayoharibu kabisa uchumi wa taifa hilo.
Rais Trump amesema Marekani haihitaji kuona vita hiyo ikiendelea kwa kuwa imekua ikisababisha maafa makubwa ya raia na wanajeshi pasipo sababu za msingi hivyo ni lazima vita hiyo iishe haraka.
Je Putin atakubali mpango huo?
Chanzo cha habari telegraph.